Majimaji mtihani mpya kwa Yanga

Muktasari:

Mabingwa watetezi wa mashindano hayo Simba tayari wameshatolewa na kuacha vita ya kusaka ubingwa huo wa Yanga, Azam na Singida United

Dar es Salaam. MABINGWA wa zamani wa kombe la FA, Yanga watalazimika kupambana na hali yao baada ya kupangwa na Majimaji katika michuano hiyo huku mchezo huo ukitarajiwa kupigwa kwenye dimba la Majimaji, Songea ambako rekodi haziwabebi kabisa Wana Jangwani hao.

Katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, Yanga imewahi kushinda kwenye uwanja huo mara moja tu, mzimu ambao huenda ukawapa ugumu kwenye mechi hiyo ya hatua ya 16 bora.

Katika mechi nyingine, KMC imepangwa na Azam, Singida na Polisi Tanzania, Stand United na Dodoma FC, JKT Ruvu na Ndanda, Prisons na Kiluvya United, Mbao na Njombe Mji huku Buseresere ikiwa nyumbani kucheza na Mtibwa Sugar.

Makocha wanena

Kocha wa Mtibwa Sugar Zubery Katwila alisema mechi dhidi  ya Buseresele itakuwa ngumu kwao kwani timu hiyo iliweza kuwatoa wapinzani wao Kagera Sugar katika hatua iliyopita.

"Buresere ni timu ya ligi daraja la tatu, ilianza mashindano haya tangu hatua ya awali lakini imeendelea kuwepo hadi sasa kwa kufanya vizuri kwahiyo tutachukulia hiyo kama changamoto ili kupata ushindi katika mechi ambayo tutacheza kwao," alisema Katwila.

Kocha wa Dodoma Jamuhuri Kihwelo 'Julio' alisema anawaheshimu Stand United kwa kuwa wapo ligi kuu lakini watafanya maandalizi makali kama walivyofanya dhidi ya Mwadui ili kuhakikisha wanapata ushindi.

"Kama nilivyopata ushindi kwa Mwadui hata Stand nao itakuwa hivyo hivyo kwani nawajua vizuri wala hawatanisumbua," alisema Julio.

Kocha wa Majimaji Habibu Kondo alisema kwanza watacheza na Yanga mechi ijayo kwenye ligi na mapungufu ambayo watayaona hapo ndio watayafanyia kazi ili kupata ushindi na kusonga katika FA.

"Tunawaheshimu Yanga ni timu kubwa lakini mechi ya FA, tutakuwa nyumbani tunaweza kupata matokeo mazuri na kusonga katika hatua inayofaata," alisema Kondo.

"Nawaheshimu Azam ni timu kubwa na wapo vizuri lakini hata sisi pia tuna wachezaji wazuri na tumeshika nafasi ya kwanza katika kundi letu kwahiyo mechi itakuwa nzuri na ambaye atacheza vizuri atapata ushindi," alisema Felix Minziro kocha wa KMC ambayo itacheza na Azam.