Bi Mwanahawa Ally awainua Wazungu kucheza mduara Sauti za Busara

Zanzibar. Matona's  Cultural  Group imefanya imekata kiu ya mashabiki  mbalimbali wakiwamo Wazungu baada ya  kutumbuiza katika Tamasha la Sauti za Busara 2018 lililofanyika Ngome Kongwe Visiwani Zanzibar jana Alhamisi usiku.

Bendi hiyo inayoongozwa na mtoto wa marehemu Issa Matona, aitwaye Mohamed, huku akisaidiwa na nguli wa muziki huo Bi Mwanahawa Ally na Patricia Hillary.

Bi Mwanahawa na Patricia waliipata nafasi ya kuzungumza na MCL Digital  kuhusu onyesho la Tamasha la Sauti za Busara na kusema kwamba: " Ni mara yangu ya pili kushiriki katika tamasha hili la Sauti za Busara, naona kuna utofauti mkubwa yaani katika tamasha hili wenyeji wachache ila wageni ni wengi tofauti na kipindi nilichowahi kuja kutumbuiza miaka mingi iliyopita.

"Sijajua kama muda ni bado au kwa wenzetu wa nje ya nchi ndio wamepata kulielewa zaidi tamasha hili, ila inapendeza sana na nimefurahi kuona Wazungu wanacheza muziki wetu wa taarabu asilia," alisema Bi Mwanahawa.

Kwa upande wa Patricia yeye alisema "Ni mara yangu ya pili kuja kutumbuiza katika tamasha hili la Sauti za Busara, nimefarijika sana kuona mashabiki damu zao hazijalala. Kweli tamasha hili wamejiandaa vizuri na sijaona mapungufu yeyote zaidi ya kufurahia Wazungu wakicheza taarabu inapendeza sana," alisema Patricia Hillary