Tujaribu tena kuwekeza kwenye masumbwi, yanaweza kututoa

KWA miaka kadhaa sasa soka imeendelea kuwa pendwa nchini ukijizolea mashabiki wengi kila kona.

Uwepo wa timu kongwe za Simba na Yanga ambazo pia ndizo zenye mafanikio zaidi kwenye soka la Tanzania umesaidia kunogesha mchezo huo ambao sasa unashika namba moja nchini kwa kuwa na mashabiki wengi.

Kutokana na mashabiki wengi kuutolea macho mchezo huo wa soka macho, michezo mingine imekuwa ikipata wakati mgumu nchini.

Michezo mingine kama Kikapu, Netiboli, ngumi, riadha na mingineyo imekuwa na sapoti ndogo kutokana na mashabiki wengi kulitazama zaidi soka.

Kwa siku za karibuni kidogo, riadha imeanza kuja juu hasa baada ya Alphonce Simbu kushinda medali ya shaba katika mashindano ya dunia mwaka jana.

Riadha sasa imejizolea umaarufu mkubwa hadi kujikuta ikishika vichwa vya habari za michezo pale ilipokuwa ikijadiliwa kama Simbu ajumuishwe kwenye kikosi kinachokwenda kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola ama la.

Ni wazi kwamba kama watu wa riadha wataweka nguvu kubwa, basi wanaweza kufika mbali na kupata mashabiki wengi.

Kwa upande wa mchezo wa ngumi maarufu kama masumbwi, umekuwa ukipanda na kushuka lakini siku za karibuni ni kama umeshuka zaidi.

Kwa miaka ya karibuni mchezo huo umekuwa ukibebwa na Fransis Cheka ambaye mara nyingi anatajwa kama bondia namba moja nchini.

Kwa siku za karibuni Cheka pia ameanza kushuka hivyo kusababisha mchezo huo uendelee kupoteza mvuto nchini.

Mabondia wengine waliopo sasa kama Ibrahim Class, Dulla Mbabe, Mohammed Matula, Cosmas Cheka na wengineo bado wameshindwa kujipambanua na kuwa mabondia wakubwa nchini.

Mchezo huo kwa sasa umekuwa na msisimko mdogo tofauti na kipindi cha nyuma ambapo wakali kadhaa kama Maneno Oswarld, Rashid Matumla, Mbwana Matula, Nassoro Michael na wengineo walikuwa na umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi.

Kwa miaka ya karibuni pia mbali na Cheka, mabondia wengine kama Fransis Miyeyusho, Mada Maugo na marehemu Thomas Mashali waliweza pia kuupandisha mchezo huo japo haukufika pale panapotakiwa.

Ni ukweli usiojificha sasa juhudi za makusudi zinahitajika ili kuunyanyua mchezo huo ambao umewatajirisha watu wengi duniani.

Pamoja na kwamba soka ndiyo mchezo pendwa nchini, bado tunaweza kuufanya mchezo wa masumbwi kuwa wenye mvuto kama nchi nyingine duniani zilivyofanikiwa.

Mfano nchini England licha ya kwamba Ligi yao imekuwa na msisimko wa kipekee, bado mabondia kadhaa kama Antony Joshua wamekuwa wakitamba duniani.

Nchini Marekani licha ya mpira wa kikapu kuwa na mashabiki wengi zaidi, bado masumbwi yamekuwa na nafasi yake na ndiyo maana bondia tajiri zaidi duniani, Floyd Myweather anatokea nchini humo.

Kwa muktadha huo ni wazi kwamba tunahitaji kuweka nguvu kubwa kwenye mchezo huo hasa katika kuwajenga mabondia wenye uwezo, kuwatangaza ndani na nje ya nchi pamoja na kuwasaidia katika maandalizi ya michezo yao mikubwa.

Hawa hawa wakina Dulla Mbabe wanaweza kuwa wakubwa endapo tutafanikiwa kuwatangaza vizuri, kuwasaidia katika maandalizi ya mapambano yao pamoja na kuyatangaza.

Pia, watu wanaohusika na masumbwi nchini wafanye juhudi sasa kusaidia mchezo huo uruke moja kwa moja kwenye televisheni kwani hilo litasaidia kuvuta mashabiki wengi zaidi nchini.

Haiingii akilini kwamba hadi leo mchezo huo unachezwa kwenye Uwanja wa Taifa na kuishia hapo hapo enzi hizi na vituo vya televisheni nchini vimejaa kama njugu.

Tunapenda kuwashauri wadau wa mchezo huo kwa namna moja ama nyingine kukaa na kujitathmini kuona namna wanavyoweza kuubeba tena mchezo huo ili uweze kuwa mkubwa nchini.

Siku zote Watanzania wanapenda michezo na tunaamini kuwa endapo ngumi zitawekwa kwenye eneo sahihi, utachukua nafasi kubwa na kushindana hata na soka, kikapu na netiboli. Kinachotakiwa ni kujipanga na kuhakikisha kila kitu kinasimama.