Waogeleaji ishu ni bwawa au kuna kingine?

Monday May 14 2018

 

By IMANI MAKONGORO

HII ya waogeleaji kali ya mwaka jamani! Si unakumbuka wiki iliyopita timu ya Tanzania ilikuwa kule Morocco kwenye mashindano ya dunia ya wanafunzi wa sekondari? Sasa bwana unaambiwa hadi bwawa la kuogelea liliwatoa ushamba mashindanoni.

Kocha aliyeambatana na timu hiyo, John Belela anakwambia kitendo cha waogeleaji kutua Morocco na kuona bwawa la kuogelea la mita 50, kila mmoja alishangaa kwani bwawa kama hilo hawajawahi kuliona.

“Walishazoea mabwawa ya mita 25 ambayo ndiyo yanatumika hapa nchini, lakini hayatambuliki kimataifa, hivyo waogeleaji walioenda Morocco ilikuwa mara yao ya kwanza kushiriki mashindano hayo walikumbwa na hofu walipoona bwawa hilo,” alisema Belela.

Alisema kitendo cha kukosa mabwawa ya mita 50 ambayo ndio yanayotambulika kimataifa ni pigo kwani waogeleaji wanakuwa katika mazingira magumu wanapokwenda kuchuana nje ya nchi.

Hata hivyo, timu hiyo haikurejea nchini mikino mitupi kwani ilifanikiwa kurudi na tuzo maalumu ya ushiriki.