Toto Africans yaitandika Pamba FC mabao 2-1

Muktasari:

Mchezo huo ambao ulikuwa muhimu kwa timu zote kuhitaji pointi tatu ili kujinusuru na janga la kushuka Daraja,Toto ilionekana kuwa na uchu zaidi na kufanikiwa kuondoka na ushindi huo.

Mwanza.Timu ya Toto Africans imeiangushia kipondo cha mabao 2-1 Pamba FC kwenye mchezo wa Ligi Daraja la kwanza uliopigwa leo Jumapili katika dimba la Nyamagana jijini Mwanza.
Mchezo huo ambao ulikuwa muhimu kwa timu zote kuhitaji pointi tatu ili kujinusuru na janga la kushuka Daraja,Toto ilionekana kuwa na uchu zaidi na kufanikiwa kuondoka na ushindi huo.
Toto 'Wanakishamapanda' walianza kucheza na nyavu dakika ya pili kupitia kwa Bernard Isdory akimalizia pasi safi ya Daniel Lukandamila,kisha Nahodha wao,Msafiri Khamis kufunga bao la pili dakika ya 16.
Kipindi cha pili kilianza kwa Pamba kubadikika tofauti na walivyokuwa awali,ambapo walichuana kusawazisha mabao hayo na kufanikiwa kupata bao moja lililowekwa wavuni na George William kwa mpira wa faulo.
Kwa matokeo hayo,Toto inabaki mkiani kwenye kundi lake C, kwa pointi 10,huku nao Pamba wakibaki nafasi ya saba kwa alama 12 baada ya kushuka uwanjani mara 12.
Ili Toto iweze kubaki kwenye Ligi,itapaswa kushinda mechi zote mbili zilizobaki,dhidi ya Rhino na Dodoma),huku pia ikiiombea Pamba dua mbaya ili ipoteze michezo yake ya mwisho dhidi ya Alliance na Rhino.

Wakati huo mkoni Shinyanga wenyeji Trans Camp wamchezea kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Alliance kwenye mechi ya Ligi Daraja la kwanza na kuifanya Alliance kupanda nafasi ya pili kwenye kundi lao C kwa pointi 22 sawa na Dodoma, lakini wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
Mabao ya Mchembe Maganda dakika ya 8 na  Dickson Ambundo dk ya 34 yametosha kuwanyamazisha Trans Camp katika dimba lao la nyumbani.