Hawa netiboli wametutia aibu jamani

Monday May 14 2018

 

UKISIKIA fedheha, basi ndio hii iliyozikuta timu za Tanzania za netiboli zilizoshiriki mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki pale kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam.

Tanzania imeishia kuwa mwenyeji tu, ikiachia vikombe vyote kuanzia lile la mshindi wa kwanza hadi wa tatu kwenda Uganda na kama haitoshi eti hadi timu ya Uhamiaji ilishindwa kushiriki kwa kisingizio cha ukata.

Unaambiwa kwenye mashindano hayo, Uganda ilitawala kama inacheza nyumbani na kwa taarifa tu timu ya kwanza hadi ya tatu zote za Uganda.

“Tulizidiwa, wenzetu walionekana kujipanga na walichokipata ndiyo matunda ya maandalizi yao,” alisema Katibu Mkuu wa Chaneta, Judith Ilunda saa chache baada ya Prisons Uganda kutawazwa kuwa mabingwa wa taji hilo.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na NIC ya Uganda na ya tatu ilienda kwa Polisi Uganda huku wenyeji waliowakilishwa na JKT Mbweni, Jeshi Stars, Polisi Morogoro na Dar kombaini ya wanaume wakitoka kapa.