Cheka bwana, eti anamuiga Tyson

Monday May 14 2018

 

By IMANI MAKONGORO

UNAIKUMBUKA ile staili ya nguli wa zamani wa dunia wa ndondi wa uzani wa juu, Mike ‘Iron’ Tyson aliyekuwa na rekodi tamu ya kumaliza mapema tu mapambano yake? Sasa bwana juzi Jumamosi bondia namba moja nchini wa uzani wa Super Middle, Francis Cheka amemuiga.

Cheka aliibuka na staili hiyo alipozichapa na Mmalawi, Libeni Masamba pale kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma ambapo kuna mashabiki walifika uwanjani lakini hawakubahatika kushuhudia pambano kwani liliisha mapema.

Ilikuwa hivi. Pambano hilo lilichezwa kwa dakika nne tu mchezo ukawa umeisha, sio kama ndio ilipangwa iwe hivyo, la hasha! Masamba alipigwa kipigo hevi cha KO dakika ya kwanza tu ya raundi ya pili mchezo ukaisha japo ilipangwa wazichape raundi nane.

“Masamba hakuwa mbaya alicheza vizuri, lakini maandalizi niliyokuwa nimeyafanya ilikuwa ni lazima nishinde,” alisema Cheka jana na kuendelea kusimulia kipigo hicho kilivyokuwa.

“Ilikuwa ni ‘timing’ alirusha ngumi ya kulia nikakwepa lakini kabla hajakaa sawa nikamrudishia kwa haraka konde la kushoto alipojaribu kukwepa akakutana na jingine la kulia lililompata sawia kidevuni akadondoka chini hakunyanyuka tena,” alisema Cheka.

Siku hiyo Mada Maugo ambaye naye alitarajiwa kucheza hakucheza huku mwenyewe akieleza alichelewa kusaini mkataba wa pambano hilo.

Baada ya pambano hilo, Cheka anakwambia sasa anaelekeza nguvu kwenye pambano la kuwania ubingwa wa dunia litakalopigwa siku ya Eid Pili mkoani Mtwara na bondia wa Ufilipino.